In lieu of an abstract, here is a brief excerpt of the content:

xxv UTANGULIZI Katika safari yangu mojawapo nilipokwenda nyumbani Mombasa kutoka huku Ulaya, mkusanyaji wa mashairi haya, Sharif Abdurrahman Saggaf Alawy (au, Maallim Saggaf, kama tumwitavyo baadhi yetu), alinikuta barabarani. Papo hapo akanishika mkono na kunichukua mpaka nyumbani kwake. Tulipofika tu, akanikabidhi mijalada miwili ya miswada ya mashairi ya washairi wa kale wa Pemba. Muswada mmoja ulikuwa na mashairi ya washairi mbalimbali wa kale wa kisiwa hicho. Kwa mfano, washairi kama Abdalla Mwinyombe Mbawara, Hemedi bin Khatoro (Sungura), Abdalla bin Salim Busaidy (Paka Shume), Mayasa binti Nasoro, Juma Yakuti Mnindi, Ali bin Mbaruk al-Mazruiy, na wengineo kadhaa. (Katika muswada huu yalikuwamo pia mashairi machache ya washairi wane wa kale wa Wasini, Pwani ya Kenya: yaani Sayyid Hassan bin Nassir (Mwinyi Alawi), Ali bin Msellem, Muhammad bin Abibakar na Muhammad bin Nassir.) Na muswada wa pili ulikuwa na mashairi ya washairi wawili tu wa Pemba walioishi katika miaka ya karibu na katikati ya karne ya kumi na tisa na miaka ya mwanzo mwanzo ya karne ya ishirini. Washairi wenyewe wakijulikana zaidi kwa majina ya Kamange na Sarahani. Nilipomwuliza niifanyeje miswada hii, Maallim Saggaf akanijibu, “Ifanye utakavyo!” Nikatambua kwamba asema nami kikuu. Basi, kitabu hiki chatokana na huo muswada wa mashairi ya Kamange na Sarahani. Na ni matumaini yetu kwamba baada ya kitabu hiki, mashairi yaliyomo katika huo muswada wa pili nayo pia yatachapishwa. Kama ilivyoelezwa kwa urefu katika Dibaji, mashairi yaliyomo humu yalikusanywa na kuhifadhiwa na Maallim Saggaf zaidi ya miaka arubaini iliyopita alipokwenda Pemba. Baadhi ya mashairi hayo yalikuwa yameandikwa katika madaftari, na mengineyo yalipatikana kutoka kwa watu waliokuwa wameyahifadhi nyoyoni. Nilipokabidhiwa, ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuiona miswada hii; lakini haikuwa ni mwanzo kusikia habari zake. Kwani kabla ya hapo, kiasi cha miaka thalathini iliyopita, nilikuwa nikijua kwamba miswada hii ikitafutiwa wachapishaji.Lakini,yaonyesha,wachapishajihawakuwanahamunayo.Sababu mojawapo, labda, ilikuwa ni ukubwa wa miswada yenyewe. Na, kutokana na sababu hiyo, wachapishaji walifikiri kwamba si wasomaji wengi watakaoweza kukinunua kitabu kitakachochapishwa; kwa ajili hiyo, hakitakuwa na faida ya kibiashara. (Na hapa ndipo mtu aonapo jinsi ilivyo muhimu kuwa na mashirika ya uchapishaji ambayo lengo lao kuu la pekee si kuweka faida ya kifedha mbele kwa kila kitabu kinachochapishwa, lakini vile vile kufikiria faida kubwa ya kusherehekeanakuhifadhiurathiwatamadunizetu,kwaajiliyakizazikilichoko, na haswa kwa ajili ya vizazi vijavyo. Kwani thamani ya utamaduni - na fasihi ya watu wowote ni sehemu ya utamaduni wa watu hao - haikadiriki kifedha.) xxvi Kale ya Washairi wa Pemba: Kamange na Sarahani Mara ya pili niliposikia habari za miswada hii, na kwa mara ya kwanza kuyasikia na kuyaona baadhi ya mashairi yaliyomo humu, ilikuwa ni katikati ya miaka ya thamanini. Wakati huo nilikuwa nafanya kazi katika Idhaa ya Kiswahili ya BBC, London. Katika muda wote wa miaka sabaa nilipofanya kazi hapo nilikuwa na kipindi changu cha kila wiki kuhusu sanaa, kilichoitwa Utamaduni. Bwana Ali Abdalla El-Maawy - ambaye baadaye Maallim Saggaf alimshirikisha katika kuyashughulikia mashairi haya - alipata safari ya kuja London, na tukazungumza katika kipindi hicho kuhusu washairi hawa wawili, Kamange na Sarahani, pamoja na kufanya uchambuzi wa baadhi ya mashairi yao. Mashairi hayo yakanipendeza sana, na nikasikitika kwamba hayakuwa yamepata bahati ya kuchapishiwa kitabu. Lakini jambo haliwi ila kwa wakati wake. Kwa hivyo, baada ya zaidi ya miaka thalathini kupita, na baada ya Maallim Saggaf kunikabidhi miswada hii, na kwisha kuisoma na kuiona hazina kubwa ya ushairi wa Kiswahili iliyomo katika mashairi haya, nikaanza kuushughulikia muswada wa kitabu hiki. Jambo la kwanza nililolifanya lilikuwa ni kuutayarisha na kuupanga upya muswada wenyewe, kwa namna ambayo mchapishaji hatatishika na huo ukubwa niliodhani kwamba ndio uliowafanya wachapishaji wakaona uzito kufikiria kuuchapisha. Wakati nilipokuwa nikiifanya kazi hiyo, kila mara nilipokwenda Mombasa nilikuwa nikikutana na kuzungumza kwa vipindi virefu virefu na Maallim Saggaf, ili kupata maelezo zaidi kuhusu mashairi yenyewe, watunzi wake na pia maelezo ya watu waliomkabidhi mashairi haya. Nilipokuwa nikishughulika na uhariri wake, nilipata kumzungumzia muswada huu ndugu yangu, Walter Bgoya, Meneja wa shirika la uchapishaji la Mkuki na Nyota. Naye - na hata bila ya kutaka mwanzo kuuona muswada wenyewe - akanambia kwamba atapendelea kukichapisha kitabu hiki. Na, kwa hilo, twamshukuru yeye binafsi, na shirika lake kwa jumla, kwa uamuzi huo. Kwani, mbali na kwamba sasa mashairi haya yamehifadhika katika kitabu, faida nyengine itakayopatikana ni kwamba watu wengi zaidi sasa watajua kwamba kumbe Pemba nayo tangu hapo zamani haikuwa nyuma kwa sanaa ya ushairi1 . Hili ni jambo ambalo si watu wengi waliokuwa wakilijua kwa sababu, kabla ya kitabu hiki, hakukuwa na kitabu kilichokusanya idadi kubwa namna hii ya mashairi ya washairi wa Pemba wa kale. Kitabu pekee nikijuacho ambacho kimechapisha mashairi machache ya washairi...

Share