In lieu of an abstract, here is a brief excerpt of the content:

Sarahani 83 Japo uwe na pashao, mimi sitaki auni Kaffa tawavuwa nguo, msende mahadharani! Tuhuma na ujingao, wanenaje ya kudhani? Muwongo wa uwongoni, wewe mjita sharifu Tamati nimewaswili, munitao uwanjani Basha Ali na Fadhili, ni wavita tangu lini? Kulla nikiwakabili, watarajiya amani Muwongo wa uwongoni, wewe mjita sharifu ✳ ✳ ✳ ✳ ✳ MASIKINI HAPENDEZI Msamiati humbari humuepuka; humkimbia hondoka nikiondoka kisibu kisingizio Mtu akiwa fakiri, khaswa kwa zamani hizi Ndugu wote humbari, na jamii ya wazazi Hayo kwangu yamejiri, kuficha kweli siwezi Masikini hapendezi, nachoka jipendekeza Nachoka jipendekeza, mimi kwetu si azizi Hawawezi nifukuza, hondoka hawaniwazi Mimi kwetu nachukiza, mwadhani sipelelezi? Masikini hapendezi, nachoka jipendekeza Ingelikuwa huruma, engelifanya shangazi Na nduguze kusimama, wakazidisha mapenzi Kitu chao kuazima, wanidhani kuwa mwizi Masikini hapendezi, nachoka jipendekeza Aidha hata swahibu, kushikana maongezi Hunifanyiya sababu, kusudi ya machukizi Hunipa kulla kisibu, naona hivi machozi! Masikini hapendezi, nachoka jipendekeza Mwisho ni jirani zangu, kama meno na ufizi Kisadaka cha kijungu, peke yangu sifanyizi Na wao huomba Mngu, nizizimiye zizizi Masikini hapendezi, nachoka jipendekeza 84 Kale ya Washairi wa Pemba: Kamange na Sarahani Rabbi baba kamwondowa, kanirithisha majonzi Kaniachiya ukiwa, sina pa kuomba nazi! Wenzangu wanibaguwa, wanioneya kinyezi Masikini hapendezi, nachoka jipendekeza Tamma Rabbi aniona, mjawe si mdumzi Moyo wangu fila sina, sisikii mtumizi Japo wote kuniguna, Ilahi ndiye mlezi Masikini hapendezi, nachoka jipendekeza ✳ ✳ ✳ ✳ ✳ NJAA HAILEI MWANA87 Msamiati ndwele ugonjwa taghiliba udanganyifu hukithiri huzidi hukukama hukubana korati korti; mahakama Njaa neno thakili, siku mnayopambana Njaa ni kama ajali, na nduli hufuwatana Njaa haikai mbali, mara moja hukubana Njaa hailei mwana, nifanyeje hali sina! Njaa usipoiweza, mwemao mwatukanana Njaa japo jizoweza, katwa haiwezekana Njaa ni neno la adha, lakini hila hatuna Njaa hailei mwana, nifanyeje hali sina! Njaa ni ndwele ya mwili, wendapo mwafuwatana Njaa usiku hulali, hapo utapoiyona Njaa ikikukabili, matumbo hukorogana Njaa hailei mwana, nifanyeje hali sina! Njaa japo kula ng’ombe, sidhani mutahamana Njaa haina kiumbe, ambaye isiyemwona Njaa haina kipembe, wendapo itakubana Njaa hailei mwana, nifanyeje hali sina! 87 Shairi hili lilipatikana kutoka kwa mwanawe Sarahani, Bwana Matwar. ...

Share