In lieu of an abstract, here is a brief excerpt of the content:

Kamange 29 Kakatuwa na kasuku, wamechoka na ahadi Na teusi na chiriku, kuwondowa sina budi Na sasa amewapiku, kwa bahati na suudi Uhai wa swifridi, sipendi ndege mwingine Nalikuwa na qumuri, mwizi akanihasidi Kuona dhiki dahari, khatima nikahamidi Rabbi ameshusha kheri, kupata mwema zaidi Uhai wa swifridi, sipendi ndege mwingine Weupe wa macho yake, wadhani zabarjadi Maungo ya teketeke, hakukazana jasadi Inshallah asinitoke, nikae naye abadi Uhai wa swifridi, sipendi ndege mwingine Kaditama nimetuwa, nimewacha hodi hodi Mapenzi yetu ya sawa, amma yeye kashitadi Sasa nimepata dawa, ya kunituza fuadi Uhai wa swifridi, sipendi ndege mwingine ✳ ✳ ✳ ✳ ✳ SASA NAPATA STIMA Msamiati ghanima neema timama timamu; iliyotimu; kamili aqali ayyama siku chache jadidi (m)pya swabahi asubuhi takrima karamu lahamu nyama rihi harufu (nzuri) baqara ng’ombe ghanama mnyama mbisho hali au upande upepo unakovumia wakati chombo, kama vile jahazi au mashua, kiko baharini ukalidhalili ukalidharau adha usumbufu; mashaka adhwima tukufu hasho kiraka cha ubao au chuma kinachotumiwa kuzibia tundu au ufa katika chombo cha baharini 30 Kale ya Washairi wa Pemba: Kamange na Sarahani Rabbi Ghafuru Rahimu, amenijaza ghanima Kanipa stima Rumu, kusafiriya dawama Sultwani Muslimu, kanipa bure na wema Sasa napata stima, siudhiki kwa safari Siudhiki kwa safari, sasa napata stima Jazira na Zinjibari, yenda kwa saa timama Ulaya na Banadiri, yenda aqali ayyama Sasa napata stima, siudhiki kwa safari Stima yangu jadidi, haina maji alama Aliitaka Sayyidi, alipokuwa Mrima Alikwisha jitihadi, isende Darisalama Sasa napata stima, siudhiki kwa safari Stima yangu swabahi, hufanyiwa takrima Idadi tende na shahi, mikate ya kusukuma Lahamu hutowa rihi, ya baqara na ghanama Sasa napata stima, siudhiki kwa safari Tamma chombo na mbisho, huona adha adhwima Mara huzumbuka hasho, kwa mawimbi na mrama Ukalidhalili posho, kunde mbovu na mtama Sasa napata stima, siudhiki kwa safari ✳ ✳ ✳ ✳ ✳ NAKWITA NURU YA MJI Ewe kito almasi, mwinyi nuru ya siraji Huyo yuwaja tumisi, wa naswaha msemaji Uje kwangu turamisi, ndilo nnalotaraji Nakwita nuru ya mji, ulizae wake ngowa ................................., ................................ Akupataye kwa siri, ashinda aliyehiji Kaifa hiyo dhahiri, ambaye akuzawiji! Nakwita nuru ya mji, ulizae wake ngowa ✳ ✳ ✳ ✳ ✳ ...

Share