-
Kamange Hali Makombo
- Mkuki na Nyota Publishers
- Chapter
- Additional Information
26 Kale ya Washairi wa Pemba: Kamange na Sarahani Ewe Shekhe Sarahani, mbona mwanikaa kombo? Hino ni suhuba gani? Akhuwa mna vikumbo! Ndiyo akhiri zamani, viumbe hapana jambo Kwani mtoto kitumbo, kunyanyuwa fyuka yangu? Kunyanyuwa fyuka yangu, ni usungo ni urombo Akatowa nyama wangu, aliye ndani ya tambo Wanafunzio ni wangu, mbona wanifanya mambo? Kwani mtoto kitumbo, kunyanyuwa fyuka yangu? Salimu bin Hemedi, amejigeuza ndembo Mchana hutaradadi, kwa salamu na hujambo Usiku kama asadi, kwa jisu kuu na fimbo Kwani mtoto kitumbo, kunyanyuwa fyuka yangu? Kama mchezo mzaha, natupigane vikumbo Ndimi udil-karaha, huharikisha mitambo Jina langu simsaha, nala watu kama chambo Kwani mtoto kitumbo, kunyanyuwa fyuka yangu? ✳ ✳ ✳ ✳ ✳ KAMANGE HALI MAKOMBO Akhuwa mwaarifiwa, Pemba mbiu ya mgambo Sarahani wakhusiwa, mwenye kondo za vigambo Bahati nimejaliwa, tangu azali kitambo Kamange hali makombo, ala alichokiwinja Katwa sirambi kiganja, naapa sili makombo Nachaguwa nikiwinja, kilicho sura na umbo Dudu kome talipunja, sichi vita vya kimwambo Kamange hali makombo, ala alichokiwinja Simba ala vya kuwanda, akiyameza matumbo Shekhe ala vya kuvunda, viliwavyo na mabombo Mabigili yawapenda, wachezao kwa urembo Kamange hali makombo, ala alichokiwinja Anadi akilingana, Pemba yote na majimbo Izara kunitukana, jina kanita “mchimbo” Wema wangu aukana, hajali kunila wambo Kamange hali makombo, ala alichokiwinja Kamange 27 Kwani akhi wanichimba, sururu kwa mitaimbo? Wala mimi sitakwimba, illa tafunguwa tambo Mgema ukimgamba, hutiya mkojo tembo Kamange hali makombo, ala alichokiwinja Mchawi hatajwi jina, nitamtaja kwa fumbo Usiku kwake mchana, enda nyanyuwa mitambo Cha kutongozeya hana, mbona ahonga kifimbo? Kamange hali makombo, ala alichokiwinja Simama nitakushika, natujifunge masombo Tucheze huku twacheka, tukitukanana nyimbo Wajinga wafurahika, wakidhaniya magombo Kamange hali makombo, ala alichokiwinja ✳ ✳ ✳ ✳ ✳ TUMEZIPAZA NGOWEO Zilitupita zamani, zamani zetu si leo Twaliingiya ngomani, zumari na viapio Twangiya mabigilini, twachaguwa tutakao Tumezipaza ngoweo, hatuchezi ngoma tena! ✳ ✳ ✳ ✳ ✳ N’NA MIYADI NA MWEZI Shani mwezi utokako, unachwa na simamizi Na huko utuliyako, kunachwa na wangojezi Mtu enendaye huko, huliwa fupa na ngozi N’na miyadi na mwezi, kuutiya mkononi ✳ ✳ ✳ ✳ ✳ ...