In lieu of an abstract, here is a brief excerpt of the content:

sura ya saba CHANGAMOTO ZA KUJIFUNZA KIRAI NOMINO CHA KISWAHILI MIONGONI MWA WANAFUNZI: MCHANGO WA VITABU VYA KOZI VILIVYOIDHINISHA Leah Mwangi, Leonard Chacha Mwita na Jacktone O. Onyango Utangulizi Lugha ya Kiswahili ina hadhi ya lugha rasmi na lugha ya taifa nchini Kenya. Kwa sababu ya hadhi ya lugha hii, somo la Kiswahili hufunzwa kama somo la lazima katika shule zote za msingi na za upili nchini. Aidha, wanafunzi wengi wa Kiswahili wana lugha zao za kienyeji na kwa hivyo hujifunza Kiswahili kama lugha ya pili (L2). Ujifunzaji huu hutokea kupitia mifumo miwili mikuu: upataji lugha na ufunzaji rasmi unaofanyika darasani. Mafanikio katika ujifunzaji rasmi wa L2 huathiriwa na mambo kama vile: mbinu za kufunzia, vitabu vya kozi anavyotumia mwanafunzi, uwezo na hali ya kisaikolojia ya mwanafunzi. Katika utafiti huu, mchango wa vitabu vya kozi vilivyoidhinishwa ulitathminiwa. Vitabu hivi vilichaguliwa kwa sababu mara nyingi uwezo wa mwanafunzi na hali yake ya kisaikolojia ni mambo ya kidhahania na yalihitaji utafiti wa kitaaluma ambao ulihitaji muda mwingi na pia ulikuwa ghali kuutekeleza. Dhana ya KN ilichaguliwa kwa sababu ya uamilifu wa dhana hii katika sentensi ya Kiswahili. Hii ndiyo dhana ya kipekee ambayo ina uamilifu wa kiima na shamirisho katika sentensi ya Kiswahili. Sentensi yoyote yenye maana kamilifu huakisi kipengele hiki muhimu cha kisarufi, huku kikiwakilishwa na maneno kamili au viambishi mbalimbali. Tafiti nyingi ambazo zimefanywa kuhusu dhana hii kama vile: utafiti wa Carstens (1991), Reynolds (1989), Naswa (2003) na Olali (1997) ziliangazia kuainisha muundo na nafasi ya KN katika sentensi ya Kiswahili. UFUNDISHAJI NA UJIFUNZAJI WA KISWAHILI 93 94 miaka hamsini ya kiswahili nchini kenya Hazikuangazia suala la ujifunzaji wa dhana hii ya KN katika Kiswahili. Wanafunzi waliokuwa wakijifunza lugha hii, walionyesha kukumbwa na changamoto nyingi katika harakati za kujifunza dhana hii. Utafiti huu ulifanywa ili kubainisha changamoto zilizotokana na mchango wa vitabu vya kozi walivyotumia wanafunzi. Lengo kuu ni kutathmini mchango wa vitabu hivi katika kufanikisha ujifunzaji wa dhana ya KN katika Kiswahili. Shule tatu za upili kutoka wilaya ya Nyandarua ya Kati zilishirikishwa katika utafiti huu. Wanafunzi wa kidato cha nne walichaguliwa. Mtafiti alipitia nakala mia moja kumi na saba za wanafunzi hawa ili kubainisha yale waliyofunzwa kuhusu dhana ya KN katika Kiswahili. Aidha, nakala tatu za vitabu vya kozi vilivyokuwa vikitumiwa na wanafunzi hawa zilipitiwa. Nakala hizi ni Chemchemi za Kiswahili - kidato cha Tatu (kitabu cha wanafunzi na Mwongozo wa mwalimu), Kiswahili Kitukuzwe - Kidato cha tatu (kitabu cha wanafunzi na Mwongozo wa Mwalimu) na Kiswahili Fasaha Kidato cha Tatu (kitabu cha wanafunzi na Mwongozo wa Mwalimu). Mbinu za kufunzia dhana ya KN zilizopendekezwa Waandishi wa vitabu hivi vitatu vya kozi walipendekeza mbinu mbalimbali zitumiwe katika ufunzaji wa dhana ya KN katika Kiswahili. Kwa mfano, Wamitila na Waihiga (2004b) walitoa mapendekezo yafuatayo kuhusiana na ufunzaji wa dhana hii: • Anza kwa kuwakumbusha wanafunzi vifupi vya maneno. • Wapatie sentensi za kawaida fupi. • Kisha toa utangulizi wa kirai. • Eleza sifa za kila fungu ili iwe rahisi kutofautisha. • Endelea hivyo hadi mafungu yote ya virai yashughulikiwe. • Wafanye mazoezi yaliyomo. Mbinu iliyopendekezwa na waandishi hawa inawiana na mbinu isiyokuwa wazi kama ilivyoelezwa na Dodson (1967) na mbinu ya usanisi kama ilivyofafanuliwa na Fromkin na wengine (2011); inamzunguka mwalimu. Katika mbinu hii, wanafunzi hufunzwa kanuni za kisarufi na kutahiniwa kuhusu kanuni walizofunzwa. Mchango wao katika somo huwa haba na hili huwafanya kutoingiliana na lugha wanayojifunza kupitia unenaji. Kilicho wazi ni kuwa mbinu hii ilikuwa maarufu katika miaka ya 1960 pale ambapo unenaji wa lugha anayojifunza mwanafunzi haukutiliwa maanani. Hata [18.118.184.237] Project MUSE (2024-04-25 14:25 GMT) hivyo, katika miaka ya hivi karibuni wataalamu wa ufunzaji wa L2 wanapendekeza kuwa walimu watumie mbinu ambazo zitamwezesha mwanafunzi kuzungumza lugha anayojifunza hata katika mazungumzo ya kawaida yasiyoratibiwa (Wilkins 1972, Krashen 1981, Fromkin na wengine 2011). Fauka ya haya, mbinu hii ina athari hasi kwa wanafunzi wa L2 ifuatavyo: huwafaa wanafunzi ambao wana kiwango cha juu cha uelewa na ufahamu wa mambo. Aidha itawafaa wanafunzi ambao husoma vitabu vingi ili waweze kuboresha umilisi wao wa dhana walizofunzwa. Kwa wale ambao hutegemea tu mafunzo waliyopewa na walimu wao, huenda mbinu hii isiwafae hasa ikiwa watashindwa kuelewa mada wanayofunzwa. Kutowashirikisha wanafunzi katika somo huweza kukuza viathiri hasi miongoni mwa wanafunzi hasa wale ambao kiwango chao cha kuelewa mambo ni cha chini. Hawa hubaki nyuma na aghalabu huhisi kuwa dhana inayofunzwa ni ngumu kwao kuielewa. Viathiri hasi hivi ni pamoja na: wasiwasi, kutojiamini, kukosa motisha wa kufanya vyema, kusahau na kutomakinika wakati wa somo. Kulingana na Krashen (1987), viathiri hasi vinapokuwa juu hujenga kizingiti ambacho huzuia ujifunzaji...

Share